Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, hadhrat Ayatollah Jawadi Amuli katika maelezo yake kuhusu umuhimu wa Ziara ya Arubaini ameandika hivi:
Imam Hasan al-Askari (a.s.) amesema: Alama za muumini na Shia ni mambo matano: Kuswali rakaa hamsini na moja, kufanya Ziara ya Arubaini ya Husein, kuvaa pete mkono wa kulia, kusujudu juu ya udongo, na kutamka kwa sauti “Bismillahir Rahmanir Rahim”.
Makusudio ya rakaa hamsini na moja ni zile rakaa kumi na saba za swala za faradhi za kila siku pamoja na swala za sunna (nafila) ambazo hukamilisha upungufu wa swala za faradhi; hasa kuswali swala ya usiku (tahajjud) katika nyakati za usiku wa manane, jambo ambalo ina faida kubwa sana. Swala hizi hamsini na moja kwa namna hiyo ilivyobainishwa, ni miongoni mwa sifa mahsusi za Mashia na ni zawadi kutoka katika safari ya Mi‘iraj ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.). Huenda siri ya kusifiwa swala kwa kuhusishwa na Mi‘iraj ya muumini ni kuwa amri yake ilitoka katika Mi‘iraj na pia humuinua mwanadamu kufikia Mi‘iraj.
Umuhimu wa Ziara ya Arubaini hauko tu katika kuwa ni alama ya imani, bali kwa mujibu wa riwaya hii ziara imewekwa katika daraja moja na swala za faradhi na sunna, kwa msingi wa riwaya hii, kama ambavyo swala ni nguzo ya dini na sharia, vivyo hivyo Ziara ya Arubaini na tukio la Karbala ni nguzo ya wilaya.
Kwa maneno mengine, kwa mujibu wa kauli ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.): Kiini cha Utume wa Mtume (s.a.w.w.) ni Qur’ani na Ahlul-Bayt: “Hakika ninakuachieni vizito viwili… Kitabu cha Mwenyezi Mungu na kizazi changu Ahlul-Bayt wangu.” Kiini cha Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ambacho ni dini ya Mwenyezi Mungu, kina nguzo yake ambayo ni swala; na kiini cha Ahlul-Bayt nacho kina nguzo yake ambayo ni Ziara ya Arubaini, hizi nguzo mbili zimetajwa pamoja katika riwaya ya Imam Hasan al-Askari (a.s.), hata hivyo, jambo muhimu ni kuelewa namna ambavyo swala na Ziara ya Arubaini humfanya mtu kuwa na dini thabiti.
Kuhusu swala, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaja mafunzo mengi, Kwa mfano amesema: Mwanadamu kiasili ni mwenye kumuamini Mungu Mmoja, lakini asili yake inapokumbwa na matukio machungu huwa na huzuni kupita kiasi, na katika matukio yenye furaha huzuia mema, isipokuwa wale wanaoswali—ambao wana uwezo wa kuondoa tabia hiyo ya ukaidi wa kimaumbile na kuiepuka pupa, huzuni isiyo na subira, na ubinafsi wa kuzuia mema—na wakawa miongoni mwa wenye kustahiki rehema maalum za Mwenyezi Mungu: “Hakika mwanadamu ameumbwa kuwa ni mwenye pupa; anapoguswa na shari huwa na huzuni kupita kiasi, na anapoguswa na kheri huwa mchoyo, isipokuwa waswaliji.”
Vivyo hivyo, Ziara ya Arubaini humwondoa mwanadamu katika pupa, huzuni kupita kiasi, na ubinafsi wa kuzuia mema, na kama ilivyosemwa, lengo kuu la Kiongozi wa Mashahidi (a.s.) lilikuwa ni kuwafundisha na kuwatakasa watu, katika njia hiyo alichukua hatua kupitia kauli na vitendo, na pia kwa kutoa damu yake yenye thamani kubwa—ambayo huunganisha njia hizi zote ni miongoni mwa sifa mahsusi za kipekee za Bwana huyo (a.s.).
Ustawi wa akili katika mwanga wa harakati ya Husayni, uk. 227–229
Maoni yako